Jenerali Brice Oligui Nguema anatarajiwa kuapishwa leo, Septemba 4, 2023 kuwa Rais wa Mpito akichukua Madaraka baada ya kupindua Utawala wa Familia ya Bongo uliodumu kwa miaka 55 nchini humo
Jenerali Nguema aliongoza Mapinduzi ya Kijeshi, Agosti 30, 2023 dhidi ya Rais Ali Bongo Ondimba aliyetawala Nchi hiyo kuanzia Mwaka 2009
Viongozi hao wa mapinduzi walisema wamevunja taasisi za taifa, kufuta matokeo ya uchaguzi na kufunga mipaka, na baadaye wakaongeza kuwa wameamua kuzifungua tena.
Nchi nyingine hazijamtambua Oligui kama kiongozi halali wa Gabon na anakabiliwa na shinikizo la kueleza mipango yake ya kurejesha utawala wa kiraia.
Oligui aliinuliwa kwa ushindi na wanajeshi wake kufuatia tangazo la mapinduzi hayo, na siku chache baada ya hapo ameonekana akiwa amezungukwa na majenerali na kanali.
Amerudia ahadi yake ya kuandaa “chaguzi huru, za uwazi, za kuaminika na za amani”, bila kutaja ni lini utafanyika lakini akisema ni lazima kwanza katiba mpya ipitishwe kwa kura ya maoni.
Siku ya Ijumaa, aliapa kuunda taasisi zaidi za kidemokrasia zinazoheshimu haki za binadamu, lakini akasema ataendelea “bila haraka”.
Kikosi cha upinzani cha zamani kinamtaka Oligui kukabidhi madaraka, lakini watu wengi nchini Gabon wanaonekana kufurahishwa na kupinduliwa kwa ukoo wa Bongo, huku sherehe zikifanyika katika mitaa ya mji mkuu Libreville na kitovu cha kiuchumi cha Port-Gentil.
Rais wa zamani Bongo alikuwa anataka muhula wake wa tatu madarakani baada ya kuingia madarakani mwaka 2009 kufuatia kifo cha babake Omar, ambaye alitawala Gabon kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miaka 40.