Jeshi la Israel limetangaza kuwa limemkomboa mwanajeshi aliyekuwa ameshikiliwa mateka na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas katika Ukanda wa Gaza, mamlaka ya Israel imesema.
Usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu “askari Ori Megidish amekombolewa, wakati wa operesheni ya ardhini, baada ya kutekwa nyara na kundi la kigaidi la Hamas mnamo Oktoba 7,” iimebainisha idara ya usalama wa ndani na jeshi la Israeli katika taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari.
Mapigano makali yanaripotiwa huko Gaza kati ya jeshi la Israel na Hamas. Operesheni ya ardhini inaendelea katika eneo la Palestina. Mapema siku ya Jumatatu, Hamas pia ilitoa video inayoonyesha wanawake watatu wakionyeshwa kama mateka, kulingana na mwandishi wetu mjini Jerusalem, Michel Paul.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema jeshi la Israel limekuwa likisonga mbele “kimbinu” katika Ukanda wa Gaza katika siku ya 24 ya vita kati ya Israel na Hamas. “IDF imepanua uingiaji wake wa ardhi katika Ukanda wa Gaza, inafanya hivyo katika hatua zilizopimwa na zenye nguvu sana, ikiendelea kwa utaratibu hatua kwa hatua,” amesema katika ufunguzi wa mkutano wa baraza la mawaziri.