Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya hapa nchini limefanikiwa kukamata Tani 13.717 za dawa za kulevya pamoja na Watuhumiwa 4987 katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Akitoa taarifa hiyo Mkuu wa kitengo cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi, Amon Kakwale amesema katika kipindi cha kuanzia January hadi Juni 2023, kitengo hicho kilifanikiwa kukamata kiasi cha Kilogramu 9,358.77 sawa na Tani 9.36 za dawa za kulevya aina ya bangi.
“Tani 4.357 za mirungi, kilogramu 1.86 za Heroin pamoja na gramu 220.05 za Cocaine zilikamatwa na ekari 105.25 za mashamba ya bhangi na mirungi yaliteketezwa”
Katika hatua nyingine ACP Kakwale amesema Operesheni hiyo ilifanikiwa kukamata Watuhumiwa 4983 ambapo kesi 3784 zilifunguliwa na kesi hizo zipo katika hatua mbalimbali Mahakamani.
Mkuu huyo ametoa onyo kali kwa wanaoendelea kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wakijihusisha na vitendo hivyo.