Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limewatia nguvuni watu 29 wakituhumiwa kujihusisha na ramli chonganishi maarufu kama Kamchape au Lamba Lamba wakiwemo waganga wa kienyeji na wawezeshaji wao wakitajwa kuwa chanzo cha migogoro, ukatili wa kijinsia, udhalilishaji na uvunjifu wa amani katika jamii.
RPC Kigoma ACP Filemon Makungu amesema wamewashikilia watu hao kutoka katika mtaa wa Kalalangabo Wilayani Kigoma wakiwa katika zoezi maarufu Kamchape la kutafuta watu wanaodaiwa kujihusisha na imani za Kishirikina.
Ikiwa ni takribani wiki moja imepita tangu Mkuu wa wilaya ya Kigoma Kupiga marufuku zoezi la Kamchape au Lambalamba katika Kijiji cha Bitale Wilayani Kigoma,sasa watu hao wameibukia katika eneo lingine la Wilaya hiyo kuendelea kutekeleza adhima yao yakudai kuwatafuta wachawi.
Filemon Mkungu kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma anasema wamewashikilia watu hao katika operesheni maalumu ya kuondoa zoezi hilo ambalo mwezi Juni raia mmoja alifariki dunia kufuatia ghasia zilizohusisha wananchi wanaounga mkono vitendo hivyo na Polisi walipokuwa wakijaribu kudhibiti au kutaka kuwatia nguvuni wahusika katika Kata ya Ilagala wilayani Uvinza.
Wakati serikali ikikabiliana vikali na vitendo hivyo mambo ni tofauti kwa wananchi kwani wamedai suala hilo linapaswa kuhalalishwa ili kumaliza vitendo vya kishirikina ambavyo vimekuwa kikwazo katika maeneo yao.
Polisi Kigoma wameendelea kusisitiza wataendelea kutafuta watu ambao wanajihusisha na zoezi hilo la kutafuta watu wanaodaiwa kujihusisha na imani za kishirikina.