Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga limesema limekamata silaha aina ya Pistol Browning (Bunduki) ikiwa na risasi 12 ambayo ilitelekezwa na mmiliki wake chooni katika shule ya Savana Plains iliyopo kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga huku mliki wa silaha hiyo bado hajapatikana.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP. Janeth Magomi, amewataka watu wote wanaomilikishwa silaha za moto kwa mujibu wa sheria kutunza silaha hizo ipasavyo ili zisilete madhara kwa jamii kutokana na uzembe.
Aidha kupitia misako na doria za kipolisi zimekamatwa jumla ya gramu 2,205 pamoja na kete 61 za dawa za kulevya aina ya bangi, pikipiki 11 zenye makosa ya kihalifu pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika kupigia ramli chonganishi.
Haya yanajiri kupitia opareshi za jeshi la Polisi zilizofanywa ndani ya mwezi mmoja uliopita, huku wito ukitolewa kwa wananchi pamoja na madereva wa vyombo vya moto kuendelea kutii sheria katika kipindi hiki cha kuelekea siku kuu za mwisho wa mwaka.