Maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini wametakiwa kuzingatia mashariti yaliyopo kwenye kiapo cha Ahadi ya uadilifu pamoja na sheria za Nchi.
Wito huo umetolewa na Katibu ukuzaji wa Maadili, Bw. Waziri Kipacha aliyemuwakilisha Kamishna wa Maadili wakati akiongoza kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa maafisa wandamizi wa Jeshi la Polisi 155 ambao wamepandishwa vyeo mbalimbali na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hafla imefanyika makao makuu ya Polisi Dodoma, tarehe 19 februari, 2024 na kuhudhuriwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura.
Bw. Kipacha ameeleza kuwa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kimeanzishwa ili kuongeza nguvu kwenye sheria, kanuni na maadili yaliyopo.
“Nimesikia wimbo wa maadili kutoka Jeshi la Polisi ni wimbo ambao umegusa mambo mengi yaliyopo kwenywe kiapo hivyo mambo hayo mkizingatia yatawasaidia katika utendaji wenu wa kazi kila siku kwa kuzingatia maadili, sheria na kanuni.” Bw. Waziri Kipacha.
Bw. Kipacha amewataka maafisa hao wa jeshi la Polisi kutambua kuwa kiapo ni dhamira ya ndani inayowaongoza kuwa waadilifu kwa kuzingatia misingi ya maadili na mikakati ya mapambano dhidi ya Rushwa.
“Sisi tunaimani na Jeshi la Polisi kuwa na nidhamu ya hali ya juu tunategemea maafisa muliokula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu muwe mfano kwa viongozi wote kwa kuzingatia uadilifu.” Bw. Waziri Kipacha.