Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) limekomboa vijiji vinne, ambavyo vilikuwa ngome za genge la kigaidi la al Shabab katika eneo la kusini-magharibi mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Wizara ya Ulinzi ya Somalia imesema kwenye taarifa yake iliyoripotiwa jana kwamba, wanajeshi wa nchi hiyo wamechukua udhibiti wa vijiji vya Dudumale, Bulo-Kajor, Abagbeday na Elgaras katika mji wa Hudur baada ya mashambulizi yaliyoashiria kuanza awamu ya pili ya kampeni ya serikali ya kupambana na magaidi wakufurishaji wa al Shabab.
Sehemu moja ya taarifa hiyo iliyotolewa Moghadishu, mji mkuu wa nchi hiyo imesema: “Jeshi la Taifa la Somalia limechukua udhibiti wa vijiji vilivyokuwa vinakaliwa kwa mabavu na Khawarij (ikikusudia al Shabab).”
Taarifa hiyo pia imesema: “Huu ni mwanzo wa awamu ya pili na hatua madhubuti ya kurejesha usalama kwa jamii zetu.”
Wizara hiyo vilevile imesema kuwa, vikosi vya serikali vimerejesha amani na usalama katika vijiji vilivyokombolewa ambako magaidi wa al Shabab walikuwa wamejificha na kuwatia hofu wananchi wa eneo hilo.