Jeshi la Sudan limewaachilia wanaharakati wawili walilokuwa wamewashikilia kwa tuhuma za kuunga mkono mahasimu wa kijeshi wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF).
Wanaharakati hao walizuiliwa siku ya Jumapili walipokuwa wakiendesha ambulensi “iliyoibiwa”, kulingana na jeshi.
Katika taarifa, jeshi lilisema liliwaachilia Jumatatu baada ya kubaini utambulisho wao.
Wanaume hao wawili waliripotiwa kunyolewa nywele zao kabla ya kuachiliwa.
Jeshi liliwataka wanaharakati “kuratibu” na wanajeshi wake endapo kutakuwa na harakati kama hizo katika siku zijazo, “ili kuepusha mkanganyiko wowote”.
Wanaharakati wanaounga mkono demokrasia, wanaojulikana kama Kamati za Upinzani, walikuwa wamekanusha madai ya jeshi kuunga mkono RSF.
Wanaharakati hao walitaka wanachama wao waachiliwe, wakisema walikuwa watu wa kujitolea kuwasaidia waliojeruhiwa katika mapigano kati ya jeshi na RSF.
Kamati za Upinzani pia zimetaka kukomeshwa kwa mzozo huo ambao umeua mamia na kujeruhi maelfu.
Makundi hayo yalikuwa muhimu katika kuhamasisha maandamano ya wiki kadhaa mitaani kudai kurejeshwa kwa utawala wa kidemokrasia baada ya majenerali wanaopigana nchini Sudan kunyakua mamlaka mwaka 2019.
Wanaharakati hao wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga jeshi tangu jeshi lilipopindua serikali ya mpito inayoongozwa na raia mwaka 2021.
Takriban 80% ya hospitali za Khartoum haziwezi kufanya kazi kikamilifu au zimefungwa kabisa. Madaktari wa ndani, pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), wamesema mfumo mzima wa afya wa Sudan unaweza kuporomoka.