Mashambulizi ya anga na mizinga mjini Khartoum yalisikika siku ya Ijumaa baada ya jeshi la Sudan linalopigana na kikosi cha Rapid Support Forces kushindwa kukubaliana juu ya sitisho la mapigano licha ya kuweka nia ya dhati kuwalinda raia na kuruhusu ufikiaji wa misaada ya kibinadamu.
Kile kinachojulikana kama tamko la kanuni lilisainiwa nchini Saudia Arabia Alhamisi jioni takribani wiki moja baada ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili, ambazo zilikuwa zikishiriakiana madaraka kabla ya kutofautiana kuhusu kipindi cha mpito kuelekea kwenye utawala wa kiraia.
Mshauri wa kikosi cha RSF Moussa Khadam alikiambia kituo cha utangazaji cha Sky News Arabia kuwa kundi hilo litaheshimu misingi waliyokubaliana inayolenga kufikia sitisho kamili la mapigano. Lakini ghasia hazijapungua na jeshi halijatoa maoni yoyote kuhusu makubaliano hayo.
Tangu mapigano yazuke ghafla tarehe 15 Aprili, makundi hasimu yameonyesha dalili ndogo kuwa wako tayari kumaliza mapigano mabaya ambayo yamewaondoa maelfu ya watu na kuifanya Sudan kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mzozo huo umeudumaza uchumi wa Sudan na kuua biashara nchini humo. Na kuongeza janga la kibinadamu huku Umoja wa Mataifa ukisema siku ya Ijumaa kuwa mpaka sasa watu 200,000 wamekimbilia nchi jirani.
Hata hivyo, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes alisema alitarajia kuwa mazungumzo ya kusitisha mapigano yataanza tena siku ya Ijumaa au Jumamosi na, wakati mapatano ya awali yameshindwa kwasababu pande zote mbili zilidhani huenda zingepata ushindi wa haraka, na sasa wanaamini kwamba ushindi hautakuja kwa haraka.