Serikali ya kijeshi nchini Burkina Faso imesitisha shughuli za moja ya redio maarufu nchini humo kutokana na kile uongozi huo unasema redio hiyo ilifanya mahojiano yanayodaiwa kudharau viongozi wapya wa jeshi katika nchi jirani ya Niger.
Kwa mujibu wa waziri wa mawasiliano nchini Burkina Faso, Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo, redio Omega imezuiwa mara moja kuendelea na shughuli zake kwa kipindi cha muda usiojulikana.
Waziri huyo amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu ya masilahi ya juu ya nchi.
Redio hiyo ambayo ni sehemu ya kampuni ya mawasiliano ya Omega inayoomilikiwa na mwanahabari wa zamani na waziri wa mambo ya kigeni Alpha Barry, imesitisha shughuli zake baada ya agizo hilo la Alhamis.
Kituo hicho kilikuwa kimefanya mahojiano na Ousmane Abdoul Moumouni, msemaji wa kundi jipya nchini Niger linalotaka kurejeshwa madarakani kwa rais Mohamed Bazoum.
Rais wa Niger aliyechaguliwa kidemokrasia, aliondolewa madarakani mwezi Julai tarehe 26 na wanajeshi nchini humo.
Burkina Faso ilishuhudia mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka jana, matukio ambayo pia yameonekana nchini Niger na Mali, mataifa yanayokabiliwa na makundi ya watu wenye silaha.