Leo October 5,2018 Mahakama ya Rufaa, imetupilia mbali rufaa ya vigogo 9 wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu dhidi ya mwenendo wa kesi yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu sababu rufaa hiyo ina mapungufu kisheria.
Rufaa hiyo ni mwendelezo kutokana na kesi ya msingi ya jinai inayowakabili viongozi hao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo wanapinga uamuzi na amri mbalimbali ambazo mahakama hiyo imekuwa ikizitoa.
Awali, walifungua maombi ya mapitio Mahakama Kuu wakiiomba Mahakama hiyo iitishe jalada la mwenendo wa kesi ya msingi na kuuchunguza pamoja na amri zake ili kujiridhisha na usahihi na uhalali wa mwenendo na amri hizo.
Rufaa ya viongozi hao imesomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Eddy Fusi ambayo imeandaliwa na jopo la Majaji watatu, wakiongozwa na Mbarouk Mbarouk, Shaban Lilla na Jacbs Mwambegele.
Katika uamuzi huo, jopo hilo la Majaji walisema taarifa ya kusudio la kukata rufaa lina dosari kisheria, kwani waombaji hawakuonyesha jambo ambalo wanalikatia rufaa kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali mapitio ya kupinga uamuzi wa Kisutu.
Katika uamuzi huo, Jopo hilo la Majaji limebainisha kuwa wanakubaliana na upande wa Jamhuri kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 68(2)zinaelekeza taarifa ya kusudio la kukata rufaa lazima ianishe asili ya uamuzi au amri ambayo inakatiwa rufaa.
Kutokana na hatua hiyo, imetupilia mbali rufaa ya vigogo hao 9, pamoja na kuyaondoa maombi ya kutaka kusitisha usikilizwaji wa kesi yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu, Dk Vicent Mashinji, manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Pia wamo Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA), Esther Matiko, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 ambayo ni kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali yanayowakabili wote, huku Mbowe, Msigwa Mdee na Heche kila mmoja peke yake akikabiliwa na mashataka zaidi.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16 katika barabara ya Kawawa, Mkwajuni, Kinondoni, siku wakihitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni na kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.