March 8, 2018 stori nayokusogezea ni kuhusu Jarida la Forbes, limetoa orodha ya matajiri wa kupindukia duniani na kumtaja mmiliki wa Kampuni ya Amazon, Jeff Bezos kuwa kinara katika orodha hiyo.
Utajiri wa Bezos umepanda na kufikia dola Bilioni 112 kutoka takribani dola Bilioni 39.2 za mwaka jana. Kuimarika kwa utajiri wa Bezos katika historia, kumemuondoa mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates kutoka katika orodha hiyo kama tajiri namba moja.
Katika orodha hiyo mpya, tajiri Gates mwenye utajiri unaokadiriwa kuwa wa dola bilioni 90 mwaka huu kutoka Bilioni 86 ndiye anayeshikilia nafasi ya pili. Gates ameongoza orodha hiyo kwa miaka 18 kati ya miaka 24 iliyopita.
Miongoni mwao, kuna Mabilionea 259 wapya ambao walijipatia utajiri wao kutoka katika biashara za aina nyingi zikiwemo nguo za harusi, wanasesere wa kuchezewa na watoto na magari yanayotumia umeme.
Marekani ndiyo nchi inayodaiwa kuwa na mabilionea wengi duniani, ambapo ina mabilionea 585, ikifuatwa na China. Jimbo la California pekee lina mabilionea 144, zaidi kushinda mataifa yote isipokuwa Marekani na China.