Leo February 28, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru wafuasi 7 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka yao ya kulizuia Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yake.
Watuhumiwa hao ni, Sunday Urio, Kizito Damia, Joseph Samky, Chrisant Clemence, Wilfred Ngowi, Karim Kinyaiyasiriri ambapo wote walikabiliwa na tuhuma za kufanya fujo na kuwazuia askari polisi kufanya kazi yao.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha mashtaka pasipo kuacha shaka yoyote na siyo upande wa utetezi kuthibitisha kukana mashtaka.
Hakimu Simba amesema, hakuna shahidi hata mmoja kati ya mashahidi watatu wa upande wa mashtaka aliyethibitisha kuwaona washtakiwa wakirusha mawe kwa Polisi na kuwaziua wasifanye kazi yao.
“Baada ya kutolewa ushahidi washtakiwa walionekana wana kesi ya kujibu, ambapo walianza kutoa ushahidi wao ambao ulikuwa unafanana kuwa hawakuwepo eneo la hilo tukio na wala hawaakutenda kosa hilo,” -Hakimu Simba
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Simba amesema anawachia huru washtakiwa wote saba sababu ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuwa dhaifu.
Katika kesi hiyo ilidaiwa, January 26, mwaka 2015 huko Ubungo eneo la Riversides, washtakiwa kwa makusudi walifanya fujo kwa kuwarushia mawe askari polisi wa kutunza amani ili washindwe kufanya kazi yao.
WALIOJERUHIWA KWA RISASI MAANDAMANO YA CHADEMA WAFIKISHWA MAHAKAMANI