Leo March 13 2017 President mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete amezindua Taasisi yake ya Jakaya Kikwete (Jakaya Mrisho Kikwete Foundation) ambapo amesema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akipenda na kujihusisha na shughuli mbalimbali za maendeleo ya watu na hivyo Taasisi yake itamsaidia katika kufikia malengo yake.
Akiizungumzia taasisi hiyo Kikwete alisema kuwa, Taasisi yake ina wajumbe 9 kutoka sehemu mbalimbali duniani wenye nyadhifa na heshima kubwa katika nchi zao. Ameongeza kuwa Taasisi hiyo imejikita kusaidia jamii katika maeneo makubwa manne, maendeleo ya jamii hasa katika kujikita kuondoa umaskini, mabadiliko ya hali ya nchi na kilimo kwa wakulima wadogo.
Aidha taasisi hiyo imejikita katika huduma za afya, kutokomeza malaria na afya ya mama na mtoto. Maeneo mengine ambayo Taasisi hiyo inajihusisha nayo ni elimu kwa vijana ili kukuza vipaji vyao na kuwapa mafunzo kuhusu uongozi bora, usawa wa kijinsia na namna ambavyo Serikali inavyotoa huduma kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa Taasisi yake itaisaidia Serikali, mashirika na Taasisi mbalimbali ili kushirikiana kuwaletea maendeleo watanzania na watu mbalimbali duniani.
Dkt. Kikwete amewataja Wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya Taasisi yake kuwa ni Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Profesa Rwekaza Mukandala Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Willium Mahalu Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Tabibu cha Bugando.
Wengine ni Balozi Mwanaidi Maajar aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Abubakar Bakhresa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya Bakhresa, Genevieve Sangudi Mtaalamu wa Masuala ya kibishara ya Kimataifa kutoka Marekani.
Pia wapo Dato’ Sri Idris Jala, Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu nchini Malaysia, Balozi Charles R. Stith aliyekuwa Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania pamoja na Dkt. Carlos Lopes ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa (UNITAR).
Taasisi ya Maendeleo ya Jakaya Kikwete ilisajiliwa tarehe 17, Februari 2017, na hii ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa Bodi ya wadhamini kukutana tangu kuanzishwa kwake.
‘Kutoka 388 kufika 163 ni panga kali’- Rais mstaafu Kikwete, Bonyeza play hapa chini kutazama