Leo May 19, 2018 Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa wito kwa nchi wanachama kuchukua tahadhari ya mlipuko wa ugonjwa wa ebola ambao umethibitishwa kulipuka katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano kwa Umma wa EAC, Richard Owora imesema Wizara ya Afya ya DRC ilitangaza mlipuko wa ugonjwa huo katika majimbo matatu ya nchi hiyo.
Amesema hadi May 15 matukio 44 ya Ebola yalitolewa taarifa na vifo vya watu 19 wakiwemo watoa huduma za afya watatu.
Amesema nchi za EAC ambazo ni Tanzania, Kenya, Burundi, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini zimeweka hatua za kiusalama ikiwa ni pamoja na kuwapima afya wanaoingia kutoka DRC kwenye mipaka yote iwapo wataonyesha dalili za ugonjwa huo sanjari na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujinga na ugonjwa huo.
Taarifa hiyo imesema wagonjwa wapya wametambuliwa katika mji wa Mbandaka ulio umbali wa kilomita 150 kutoka mji wa Bikoro unaosadikiwa kuwa chanzo.
“Nchi tano kati ya sita wanachama wa EAC zinapakana na DRC, pia zimekuwa na uhusiano wa kibiashara wa karibu sana kwa kuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaovuka mipaka kila mara, zikiwemo safari za moja kwa moja za ndege kati yetu. Hali hii inatufanya tuchukue tahadhari kubwa,” amesema Owora