Leo September 17, 2018 Kimbunga kimepiga China baada ya kuua watu zaidi ya 50 Ufilipino na kupiga eneo la Guangdong ambalo ni eneo lenye watu wengi zaidi huku kikitishia kuleta madhara makubwa Hong Kong na Macau.
Kinasafiri Maili 170 kwa saa na kwa mujibu wa shirika la kutoa tahadhari za vimbunga la Marekani mwendokasi huo ni mara mbili ya Kimbunga Florence.
Kwenye pwani ya China vinu viwili ya Nyuklia, Yangjiang na Taishan vimeonekana kuwepo katika njia ya Kimbunga hicho lakini Mamlaka katika kinu cha Yangjiang imesema ipo tayari na imejizatiti kujilinda.
Kwa upande mwingine, daraja refu zaidi duniani linalokatisha baharini lenye urefu wa maili 34 lililogharimu dola za Kimarekani Bilioni 20 lipo hatarini kutokana na kukatiza kwenye Bahari ya Kusini ya China ambapo Kimbunga hicho kinapita.
Daraja hilo linalounganisha Hong Kong, Macau na Zhuhai lilitengenezwa kukaa miaka 120, kuhimili upepo wa kasi ya maili 120 kwa saa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa Kipimo cha tetemeko richa 8.