Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo amesema Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan licha ya Urais wake pia ni Mama na siku zote Mama hawezi kuwatelekeza au kuwaingiza chaka Watoto wake hivyo Rais, Serikali anayoiongoza na CCM haziwezi kuwapotosha Wananchi kuhusu mkataba wa uendeshaji wa Bandari ya Dar es salaam.
DC Jokate amesema hayo leo wakati hafla ya kuhamasisha Wananchi kuhudhuria Mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo utakaofanyika Viwanja vya Shule ya mazoezi, Korogwe, kesho July 19, 2023.
“Serikali hii iliyofanya makubwa haiwezi kutupotosha, haiwezekani yaani kwa akili tu ya kawaida, na ukizingatia CCM ndio Waasisi wa hii Nchi, CCM tunajivunia tumetengeneza Nchi kwa kushirikiana na Wananchi, ramani ya Nchi imetengenezwa na Mwl Nyerere na wenzake ambao waliunda TANU ikaja CCM sasa CCM ile leo hii ijichanganye?, haiwezekani”
“Mmeona wapi Mama akamtelekeza Mtoto wake au akawatelekeza Watoto wake? haijalishi ni hali gani ije mvua lije jua, awe na fedha asiwe na fedha Mama hajawahi kutelekeza Watoto wake, Rais pamoja na Urais wake lakini ni Mama, hawezi kutuingiza chaka na hawezi kututelekeza”
“Watatokea Watu kupotosha suala hili (la uwekezaji wa bandari) pengine kwa maslahi yao binafsi na kwakuwa wameshikwa pabaya wanadhani hili jambo la uwekezaji wa bandari likifanikiwa litakipa sifa Chama cha Mapinduzi (CCM), litampa sifa Rais wa kwanza Mwananke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia na Watu wengi hawapendi vitu vizuri vikutokee”