Rais mpya wa Liberia Joseph Boakai ameapishwa rasmi kuiongoza nchi hiyo kufuatia ushindi wake mwembamba dhidi ya nyota wa zamani wa soka George Weah katika uchaguzi wa Novemba.
Boakai, mwenye umri wa miaka 79, ameahidi kuliunganisha taifa hilo la Afrika Magharibi na kufufua uchumi wake.
Pia ametilia mkazo juu ya kuheshimiwa kwa utawala wa sheria, kupambana na ufisadi na kuleta matumaini mapya kwa raia wa Liberia kama moja ya vipaumbele vyake.
Hata hivyo, hafla hiyo ilimalizika ghafla baada ya Boakai, aliyekuwa amevaa mavazi ya kitamaduni ya Liberia, kuonyesha dalili za uchovu wakati alipokuwa akitoa hotuba yake.
Boakai mwenye umri wa miaka 79 alimshinda Weah kwa kiwango kidogo katika uchaguzi wa marudio wa Novemba, kwa asilimia 50.64 ya kura dhidi ya asilimia 49.36.
“Tunashuhudia nyakati ngumu, tunaona kutokufaulu. “Tunaona ufisadi katika maeneo ya juu na ya chini. Na-ni katika hali hizi na zinazoendana ambapo tumekuja kuwaokoa,” Boakai alitangaza katika sherehe yake ya kuapishwa.