Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli leo January 24, 2018 amemtumia salamu za rambirambi Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma kufuatia kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Robert Kisanga kilichotokea January 23, 2018 katika hospitali ya Regency Jijini DSM.
Rais Magufuli amesema Jaji Mstaafu Robert Kisanga atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa wakati wote wa utumishi wake uliojaa umakini, uchapakazi, uzalendo na ushirikiano na wengine, mambo ambayo yalimwezesha kupata mafanikio.
“Sote tunafahamu kazi nzuri alizofanya akiwa katika majukumu mbalimbali ya kitaifa, mchango wake katika kuijenga taaluma ya uanasheria baada ya Uhuru na uanzishaji wa Mahakama ya Rufani baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, kwa hakika mchango wake hautasahaulika.”-Rais Magufuli
“Nakuomba Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma unifikishie salamu zangu za pole kwa familia ya Marehemu Jaji Mstaafu Kisanga, Majaji na wanasheria wote, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu” -Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewaombea wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na amemuombea Marehemu Jaji Mstaafu Kisanga apumzishwe mahali pema peponi.
BREAKING: RAIS MAGUFULI AMETENGUA UTEUZI WA MKURUGENZI BUTIAMA