Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo March 27, 2017 amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia June 30 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam. Ripoti hiyo imewasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad Ikulu Dar es salaam.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri inayofanya na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo ili kukabiliana na mianya yote inayosababisha upotevu wa fedha za umma.
Hata hivyo Rais Magufuli amemuagiza CAG kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote ambayo inasababisha nchi kukosa mapato makubwa hususani katika misamaha ya kodi, mikataba mbalimbali na ulipaji wa kodi.
“Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka, nataka ukakague kwa kina hii sekta ya madini ili watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana sawasawa?”;- Rais Magufuli.
“Waziri Mkuu ukaongoze hicho kikao na wewe CAG uwaambie kila mmoja katika eneo lake juu ya dosari zake, sitaki kuona dosari zinajirudia zilezile kila wakati”;-Rais Magufuli.
VIDEO; Mbele ya JPM, idadi ya Meli bandarini yatajwa, Bonyeza play hapa chini kuitazama