Leo May 16, 2018 Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia pamoja na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali.
Makubaliano hayo yametiwa saini Jijini DSM na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Rais Dkt. Magufuli Profesa Palamagamba Kabuni na Mkurugenzi wa Tanzanite One Faisal Juma.
Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa kamati ya majadiliano kwa upande wa Serikali, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzanite One imekubali kulipa fidia Serikali kutokana na mambo iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu ulioleta hasara kwa Serikali.
Amesema fidia hiyo inatakiwa kulipwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili kuanzia leo na haitahusisha Kodi. Pia Kampuni hiyo Tanzanite One italazimika kulipa kodi kama kawaida inazodaiwa na Serikali na tozo nyingine zote zinazodaiwa na Serikali.
Pia Serikali imekubaliana na Kampuni ya Tanzanite One kuwa itafuata masharti yote ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa ni Watanzania tu ndio wanaoruhusiwa kuchimba madini ya Vito na pale ambapo watanzania hawana uwezo huo ndipo wanapoweza kuingia ubia na wageni.
Aidha Prof. Kabudi amesema kuhusu wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite katika eneo la Mirerani utaratibu mpya unawekwa lengo kubwa ikiwa ni kutekeleza sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inalenga madini ya vito kuwa mikononi mwa Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma amemshukuru Rais Magufuli kwa kuunda kamati hiyo ya kizalendo katika kufuatilia rasilimali za madini nchini ambapo wameweza kujadiliana na kufikia muafaka wa kulipa fidia ikiwa ni mbali na malipo yote yaliyotakiwa kulipwa serikali ikiwemo kodi.
Amesema Tanzanite One itahakikisha inafuata taratibu zote za Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kwa lengo la kuhakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha Watanzania na kwamba uvunjifu wa sheria uliofanywa na kampuni hiyo hautajirudia tena.
“Sisi kama Tanzanite One tunaihakikishia Serikali kuwa uaminifu uliotuonyesha na sisi pia kama Kampuni tutahakikisha tunakuwa waaminifu na kuwa zao hili linanufaisha taifa kutokana na imani aliyotuonyesha Rais kama wananchi wake kutupa nafasi na fursa ya kusikilizwa ili kurekebisha makosa tuliyoyatenda” amesema Faisal.
Faisal amesema Tanzanite One itahakikisha haitafanya makosa iliyofanya mara ya kwanza na hivyo kuwa mfano wa kampuni nyingine za madini kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania.