Ikiwa zimebaki siku 2 kwa Klabu ya Simba kufanya Mkutano Mkuu baadhi ya wanachama wa Klabu hiyo chini ya Bodi ya Wadhamini leo August 10, 2017 wamefungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisuttu kuzuia mkutano huo ambao umepangwa kufanyika August 13, 2017.
Zuio la mkutano huo limewasilishwa Mahakamani na Wakili wa Bodi hiyo, Juma Nassor chini ya hati ya dharula ambapo amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa wamefungua kesi hiyo wakiwashtaki wanachama ambao wanakaimu nafasi ndani ya Klabu hiyo.
Washtakiwa hao ambao wanaowakilishwa na Wakili Mutakyamilwa Philemon ni Salim Abdallah, Iddy Kajuna na Dk. Arnold Kashembe.
Wakili Nassoro amedai anaiomba Mahakama izuie mkutano huo ambao unatarajia kufanyika August 13, 2017 hadi kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa akisema>>>”Tunaomba uzuiwe kwa sababu ya maslahi ya haki, hivyo Mahakama itoe amri.”
Aidha, amedai kuwa, Bodi hiyo inapinga wanaokaimu uongozi wa Klabu ya Simba kuitisha Mkutano Mkuu na kuendelea na maandalizi ya kubadilisha klabu hiyo kutoka mfumo wa Uanachama na Bodi ya Udhamini na kuwa kampuni ya Kibiashara akisema wamepinga suala hilo, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utaratibu huo kutokubaliana na Katiba ya Simba iliyosajiliwa na RITA mwaka 1975 ambayo imeunda Bodi ya Udhamini.
Wakili Juma Nassor amedai kuwa katika suala la Kikatiba wanaokaimu hawana mamlaka, kwani kwa mujibu wa Katiba utaratibu wa mikutano upo na waliopo hawajakidhi vigezo kwani inatakiwa Makamu wa Rais wa Simba ndio aitishe huku pia kitendo hicho cha kuhamisha umiliki wa Simba ni kwenda kinyume na Bodi ya Simba ambayo hadi sasa haijafutwa.
Hata hivyo, Wakili wa washtakiwa, Philemon amedai kuwa wana pingamizi la awali kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ambapo kutokana na hatua hiyo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi kesho saa 7:30 mchana kwa ajili ya kusikiliza na kutoa uamuzi wa pingamizi hizo.