Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali mwenendo nzima wa maombi yaliyofunguliwa na Juma Magoma na wenzake ya kutaka kuundoa uongozi wa Klabu ya Yanga madalakani na pia kuweka kando tuzo na amri zote zilizotolewa katika hukumu iliyowapa ushindi wazee hao.
Aidha, Mahakama hiyo imemuaru Magoma, Geofrey Mwaipopo na Abeid Mohamed Abeid walipe muombaji ( Bodi ya Wadhamini ya Klabu ya Yanga) gharama za uendeshaji wa shauri hilo.
Uamuzi huo, ulitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga wa mahakama hiyo, wakati akitoa uamuzi wa marejeo ya shauri la maombi namba 187/2022 yaliombwa na bodi hiyo kwa madai kuwa wazee hao hawakuwa na sifa ya kufungua shauri.
Hakimu Kiswaga alisema bodi hiyo iliwasilisha maombi manne ya kuomba kufanya marejeo, ambapo mahakama imekubali matatu na moja imelitupilia mbali kwa madai kuwa halina mashiko kisheria.
Alisema kuwa sababu ya kwanza ni kwamba, bodi hiyo inadai kuwa Magoma na wenzake walipeleka maombi yao kwenye mahakama ambayo haina mamlaka ya kuyasikiza ambayo ni Mahakama ya Kisutu.
“Kutokana na maombi yao waliyoyeleta kwenye maombi namba 187/2022 ni wazi yalitakiwa kupelekwa Mahakama Kuu na sio hapa kwa sababu walikuwa wanalalamika juu ya uhalali wa uwepo wa Bodi ya Wadhamini ya Klabu ya Yanga na uongozi uliyopo sasa,”alisema Kiswaga
Alisema sababu ya pili, Mahakama inaona haina mashiko kwa sababu ili mahakama iweze kufanya marejeo hapaswi kwenda kuangalia ushahidi, suala la kwamba walitakiwa kutoa kadi za uanachama ili kuhalalisha uanachama wao ni suala la ushahidi.
Pia, alisema sababu ya tatu, Magoma na Mwaipopo walitakiwa kufungua shauri la kwa hati ya madai na sio maombi kama walivyowasilisha wao, jambo ambalo mahakama imeona ni sababu ya kuikubalia bodi hiyo kufanya marejeo ya shauri hilo.
“Sababu ya nne, baada ya mahakama kupitia kumbukumbu ya shauri namba 187/2022 imebaini kuwa Abeid alijitabanaisha kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Bodi na kwamba Fatma Karume alimruhusu amuwakilishe mahakamani jambo ambalo hakuwahi kuruhusiwa kufanya hivyo,”
“Abeid hakuwahi kupata idhini kutoka kwa mtu yeyote ya kumsimamia mahakamani na hakuweza kujibu chochote juu ya tuhuma hizi kwa maana hiyo bodi ya wadhamini na Karume hawakuwa na muwakilishi, hivyo walinyimwa haki yao ya kusikilizwa,”alisema
Hakimu huyo, alisema kwa sababu hizo mahakama inaona maombi ya marejeo yana mashiko, kwa hiyo imekubali Bodi ya Wadhamini ya Klabu ya Yanga kufanya hivyo.
“Mahakama imetupilia mbali mwenendo nzima wa maombi namba 187/2022 yaliyofunguliwa na Magoma na wenzake na kuweka kando amri zote zilizotolewa katika hukumu hiyo pamoja na tuzo iliyolewa Agosti 2,2023,”
“Na kuhusiana na gharama za shauri hili, mahakama inaamuru Magoma, Mwaipopo na Abeid wamlipe muombaji wa maombi ya marejeo ambayo ni Bodi ya Wadhamini ya Klabu ya Yanga,”alisema Hakimu Kiswaga
Ilidaiwa kuwa Novemba 6, mwaka 2022, watu wawili waljiita wanachama wa Yanga walifungua shauri, ambai ni Juma Ally (Magoma) aliyekuwa mlalamikaji namba moja na Geofrey Mwaipopo ambaye ni mlalamikaji namba mbili na wa tatu ni Jabir Katundu.
Walifungua dhidi ya Baraza la Wadhamini kama mlalamikiwa namba moja, Fatma Karume, Abeid Mohamed Abeid, ambaye ni mlalamikiwa namba tatu.
Alisema walichokuwa wakihitaji ni kuondoka kwa viongozi waliopo, na mali za klabu na timu wakabidhiwe wao, mwenendo wa shauri hilo ndiyo ambao umetupiliwa mbali.