Klabu ya Simba imekamilisha usajili wa kiungo mkabaji Thaddeo Lwanga, akiwa ni mbadala wa Gerson Fraga ambaye anamajeruhi yatakayomuweka nje ya uwanja kwa msimu mzima.
Thaddeo raia wa Uganda mwenye umri wa miaka 26 anajiunga na klabu ya Simba akitokea katika klabu ya Tanta ya nchini Misri.
Taarifa ya usajili ya mchezaji huyo iliyotolewa na klabu ya Simba SC haijaweka wazi kiungo huyo amesaini mkataba wa muda gani.
Kiungo huyo wa zamani wa vilabu vya Express FC, SCV Kampala, na Vipers FC za nchini Uganda, anajiunga na Simba SC ikiwa ni siku chache tangu Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Simba Mohamed Dewji kuweka wazi kuwa watasajili kiungo mkabaji atakae ziba nafasi ya Gerson Fraga mwenye majeruhi yatakayomuweka nje ya uwanja msimu mzima.
Fraga raia wa Brazil alipata majeruhi ya goti kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara kati ya Simba na Biashara United mchezo ambao Simba walishinda kwa mabao 4-0.
Thadeo Lwanga ni mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) tangu mwaka 2015 na ameshaichezea jumla ya michezo 19.