Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya,Reuben Mfune, amewataka watendaji wa kata, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuhakikisha wanakamilisha zoezi la anuani za makazi kabla ya April 30 mwaka huu na kuahidi kuwachukulia hatua za kisheria wale watakao kwamisha zoezi hilo.
Mfune ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara aliyoufanya katika Kata ya Ihahi na Itamboleo ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kabla ya April 30 mwaka huu na kwamba maeneo yote muhimu yaliyotengwa na wananchi yafikiwe.
Amesema ni lazima kila mwananchi ashiriki kwenye zoezi hilo la anuani za makazi kwa madai kuwa linagusa moja kwa moja maisha ya watanzania kujua idadi yao ili rasimali zitakazopatikana ziwezi kutolewa kulingana na wananchi waliopo.
Hata hivyo amesema kukamilika kwa zoezi hilo kutarahisisha shughuli za sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika ifikapo agosti mwaka huu.
“Nawashukuru sana wananchi kwa muitikio wenu kushiriki zoezi hilo inaonyesha ni jinsi gani mnatamani kupata maendeleo, nimeona vijiji na vitongoji vyenu vimepambwa na vibao vya anuani za makazi, sasa kazi kwenu watendaji wa serikali za mitaa kuhakikisha maeneo yote yaliyotengwa kufikiwa na zoezi hili yanakamilika mtendaji atakayekwamisha atashughulikiwa,” amesema Mfune.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kijiji cha Itamboleo, Samwel Kaganga ameema hadi kufikia April 20 mwaka huu zoezi la anuani za makazi katika eneo lake litakuwa limekamilika.
Aidha amewaomba wananchi wa eneo hilo kuendelea kuchangia sh. 1000 kama gharama ya utengenezaji wa vibao hivyo ambavyo vitawekwa kwenye makazi ya watu.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ihahi, Bahati Salum amesema zoezi la kuweka vibao vya mitaa na namba za nyumba limekuwa shirikishi ambapo kupitia mkutano wa hadhara wananchi walipewa nafasi ya kuchagua majina yatakayowekwa kwenye vibao hivyo.
Aidha amemuahidi Mkuu wa Wilaya kuwa zoezi hilo katika kata yake litafanikiwa kwa asilimia 100 kwa sababu wananchi wamepatiwa elimu juu ya umuhimu wa anuani za makazi kwa ajili ya maendeleo yao.