Rais wa Rwanda Paul Kagame aliapishwa Jumapili kwa muhula wa nne baada ya kushinda katika uchaguzi wa mwezi uliopita kwa zaidi ya 99% ya kura.
Viongozi kadhaa wa nchi na viongozi wengine kutoka mataifa ya Afrika walijiunga na sherehe za uzinduzi huo katika uwanja wa michezo wenye viti 45,000 mjini Kigali, ambapo umati wa watu ulikuwa umeanza kukusanyika kuanzia asubuhi na mapema.
Kagame alikula kiapo mbele ya Jaji Mkuu Faustin Ntezilyayo, na kuahidi “kulinda amani na mamlaka ya kitaifa, kuimarisha umoja wa kitaifa.”
Matokeo ya uchaguzi wa Julai 15 hayakuwa na shaka kamwe kwa Kagame, ambaye ametawala taifa hilo dogo la Kiafrika tangu mauaji ya kimbari ya 1994, kama kiongozi mkuu na kisha rais.
Alishinda 99.18% ya kura zilizopigwa ili kupata miaka mingine mitano madarakani, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi.
Wanaharakati wa haki walisema ushindi mkubwa wa mzee huyo wa miaka 66 ulikuwa ukumbusho tosha wa ukosefu wa demokrasia nchini Rwanda.
Wagombea wawili pekee ndio walioidhinishwa kushindana naye kati ya waombaji wanane, huku wakosoaji kadhaa mashuhuri wa Kagame wakipigwa marufuku.