Kaka yake Paul Pogba, kiungo wa zamani wa Manchester United, amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela, miaka miwili ikiwa imepunguzwa, baada ya kukutwa na hatia ya kujaribu kumnyang’anya kaka yake.
Mathias Pogba, ambaye pia alipigwa faini ya Euro 20,000 (£16,500), ataepuka kukaa jela na badala yake atatumikia mwaka mmoja uliosalia akiwa amevalia bangili ya kielektroniki.
Wanaume wengine watano walipatikana na hatia ya unyang’anyi na uhalifu mwingine, na kuhukumiwa kati ya miaka minne na minane katika mahakama ya Paris siku ya Alhamisi.
Paul Pogba, 31, alisema “alidanganywa na marafiki zake wa utotoni” ambao walimshikilia mtutu wa bunduki mnamo 2022 na kumtaka awape €13m (£10.8m). Alisema aliwalipa €100,000 (£82,600).
Wakili wa Mathias Pogba, Mbeko Tabula aliiambia RMC Sport hukumu hiyo ilikuwa “kali sana” na akaongeza “Nadhani tutakata rufaa”.
Mwaka jana, Paul Pogba aliiambia Al Jazeera kwamba alikuwa amefikiria kustaafu soka kwa sababu ya jaribio la unyang’anyi.