Kufuatia tamko la Waziri wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, George Simbachawene la msamaha kwa wanaomiliki silaha kinyume na sheria kwasababu mbalimbali ikiwemo kuisha muda wa kibali cha umiliki au kurithi silaha iliyokuwa ikimilikiwa na aliyefariki au sababu yeyote, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam inasisitiza kufanyika kwa utekelezaji wa kusalimishwa kwa silaha hizo kama ilivyoaagizwa tangu November 01, 2021 hadi November 30, 2021.
Polisi Kanda Maalum imesema silaha hizo zinapaswa kusalimishwa katika vituo vyote vya Polisi , Ofisi za Serikali za mitaa na kwa Watendaji wa Kata kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.
“Jeshi la Polisi linawataka wote wanaomiliki silaha kinyume na Sheria kuhakikisha wanasalimisha silaha hizo katika muda uliotolewa na muda huo utakapomalizika msako mkali wa eneo kwa eneo, nyumba kwa nyumba utafanyika ukiongozwa na taarifa za ki intelijensia lengo likiwa ni kuhakikisha wanaomiliki silaha kinyume na sherria wanakamatwa na hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi yao” ——— Jumanne Muliro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam