Kamanda wa Meli za Kivita za Russia katika Bahari Nyeusi Viktor Sokolov ameonekana kwenye mkutano katika picha zilizotolewa na wizara ya ulinzi ya nchi hiyo, siku moja baada ya Ukraine kudai ilimuua katika shambulizi la kombora.
Wizara ya Ulinzi ya Russia ilisambaza video na picha hizo jana Jumanne, zikimuonyesha Sokolov — mmoja wa maafisa wakuu wa Jeshi la Wanamaji la Russia akishiriki katika mkutano wa makamanda wa kijeshi ambao uliongozwa na Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu.
Kiev ilidai juzi Jumatatu kwamba vikosi vyake maalumu viliwaua maafisa 34 akiwemo Sokolov katika shambulizi ambalo ilidai halijawahi kushuhudiwa kwenye makao makuu ya meli za kivita za Russia katika Rasi ya Crimea wiki iliyopita.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov pia anaonekana kwenye video hiyo ya wizara ya ulinzi, akisema kwamba mashambulizi ya Ukraine hadi sasa hayajazaa matunda huku akiongeza kuwa vikosi vya kijeshi vya Ukraine vinapata hasara kubwa vitani.
Peskov alisema Marekani na washirika wake wa Magharibi “wanaendelea kuvipa silaha vikosi vya kijeshi vya Ukraine, na serikali ya Kiev inawatuma vitani wanajeshi wasio na mafunzo ambao wanauawa wakiwa wanafanya mashambulizi ya kipumbavu.”
Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umeipatia Ukraine silaha zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 43 tangu Russia ilipoanzisha “operesheni yake maalumu ya kijeshi” nchini Ukraine Februari mwaka jana.