January 27, 2020 Kamati ya Bunge ya Uwekezaji ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Raphael Chegeni, imefanya ziara katika kiwanda cha ALAF jijini Dar es salaam.
Madhumuni ya ziara hii ni kuipa Kamati hiyo uelewa zaidi kuhusu shughuli mbalimbali za uzalishaji wa bidhaa zinazofanywa na kiwanda hicho.
Tarehe 14 Januari mwaka huu, Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. Dipti Mohanty alipata mwaliko wa kuhudhuria kikao cha Kamati hiyo ya Bunge ya Uwekezaji, ambapo alipata fursa ya kuelezea mafanikio ya kampuni hiyo na changamoto mbalimbali za kibiashara.
Kamati hiyo iliipongeza ALAF kwa mafanikio makubwa iliyopata hivi karibuni, na kuahidi kuitembelea kampuni hiyo, ahadi ambayo imetimizwa leo na Mwenyekiti wa Kamati pamoja na Wajumbe wote.
Katika ziara ya leo, Kamati imepata fursa ya kutembelea kiwanda cha ALAF na kujionea hatua za uzalishaji, bidhaa na huduma mbalimbali. Pamoja na kukutana na baadhi ya wafanyakazi wa ALAF, pia walitembelea kituo cha afya kinachotoa huduma za matibabu kwa wafanyakazi na familia zao,.
Mtendaji Mkuu, Dipti Mohanty ameishukuru Kamati ya Bunge ya Uwekezaji kwa kupata muda wa kutembelea ALAF. Mtendaji Mkuu huyo ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi zake za kujenga Tanzania ya viwanda, na kuikaribisha Kamati hiyo kutembelea ALAF tena.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji, Mhe. Raphael Chegeni, alisema wamekuja kuangalia jinsi gani wanaweza kusaidia ukuwaji wa sekta ya viwanda pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa nishati ya umeme wa hakika pamoja na malipo ya VAT zinazodaiwa kutoka kwa mamalaka ya mapato TRA.