Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza serikali kwa kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini ikiwemo kuhakikisha kwamba kunakuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamati hiyo ilipofanya ziara katika viwanda vya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa lengo la kufuatilia uzingatiaji wa taratibu muhimu za usalama na afya kazini miongoni mwa waajiri nchini.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Hassan Toufiq ameipongeza serikali kwa kuwawezesha wawekezaji nchini kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija.
“Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yetu ya kawaida na tumefurahi kuona wenye viwanda tuliowatembelea leo wamepata mafanikio makubwa katika shughuli zao kwani wanafanya uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi yetu. Wawekezaji hawa wamekiri kupata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini ikiwemo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ambao wamekuwa wakiwasaidia katika kuweka mifumo ya kudhibiti ajali na magonjwa pamoja na kufanya ukaguzi wa mifumo ya umeme na mitambo ya uzalishaji jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa ufanisi wa mitambo husika pamoja na kuiweka katika hali ya usalama wakati wote,” amesema Mwenyekiti Fatma Toufiq.
Aidha, Toufiq amesisitiza kuwa uwekezaji katika viwanda ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi kutokana na faida zake zikiwemo kuzalishaji ajira nyingi, kuongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu pamoja na kuongeza pato la Taifa kupitia ulipaji wa kodi.
“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hasa kwa wawekezaji wa ndani. Tunaishauri serikali kuendelea kujenga mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ili wawekezaji wetu wazidi kukua na kuongeza mtandao wa uzalishaji wao ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu,” amesema Toufiq.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Boniface Mwita, amesema uwekezaji nchini kwa kiwango kikubwa bado unategemea nguvukazi zaidi hivyo ni muhimu kuwekeza katika mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.