Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kigoma Mjini imeipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) kwa utekelezaji mradi wa uboreshaji wa chanzo cha maji Kibirizi. Mradi huo unatarajiwa kuwawezesha wananchi wa Kijiji cha Kalalangabo kupata huduma ya maji safi,salama na ya kutosha.
Mwenyekiti wa CCM Kigoma Mjini, Mheshimiwa Ahamed Mwilima, akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, aliipongeza KUWASA kwa jitihada zake za kusaidia kutekeleza wa ilani ya chama kwa kusogeza na kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kigoma Mjini na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Mwilima alisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi kama hii, ambayo inatatua moja kwa moja changamoto za wananchi, ni kielelezo cha wazi cha watendaji katika kuendelea kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maji katika juhudi za kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Kigoma Mjini, Ndugu Sadick Kibwana, alitoa pongezi za dhati kwa Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA kwa mawazo na utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo huu wa Kalalangabo, ambao unaenda kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Awali, akisoma taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maji, Yasinta Jovin, alisema kuwa hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 80 ya kukamilika kwake, ikiwa ni takriban mwezi mmoja tangu uanze kutekelezwa, na tayari wananchi wa Kijiji cha Kalalangabo wanaendelea kutumia huduma ya maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA, Ndugu Poas Kilangi, alieleza kuwa uboreshaji wa chanzo hicho, ambao umegharimu shilingi milioni 160 za fedha za ndani, ulitokana na pampu iliyokuwa ikitumika hapo awali kushindwa kutosheleza mahitaji ya wananchi, ambao sasa wanafikia zaidi ya 2000. Pampu hiyo pia ilizama katika maji kutokana na kujaa kwa Ziwa Tanganyika.
Kilangi alitoa rai kwa wananchi kushirikiana na KUWASA katika kulinda eneo la chanzo kwa kuzuia shughuli zozote za kibinadamu ambazo zinaweza kusababisha athari na kuwanyima wananchi huduma ya maji safi na salama.