KANISA la Spirit Word Ministry lililo chini ya Askofu Dkt. Caesar Masisi wameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutenda haki baada ya uchunguzi kuonesha kuwa halina hatia.
Hatua ya Kanisa hilo kutoa shukrani kwa Serikali inakuja baada ya kufugiwa kutokana na kudaiwa kuchochea mapenzi ya jinsia moja, baada ya kusambazwa kipande kidogo cha video kwenye mitandao ya kijamii ambacho kilisababisha taharuki.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana wakati akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Askofu Dkt. Masisi alisema wamepokea taarifa ya uamuzi ambao umewaondolea shutuma na hatia .
“Tunaishukuru Serikali yetu, chini ya uongozi wa Rais Samia, imetenda haki dhidi yetu uchunguzi umeonesha kwamba hatuna hatia, ni mitandao ya kijamii ilipotosha lengo la ukweli, kwani ilionyesha tu sehemu ndogo ya video kutoka video kuu. Ilikatwa na kusambazwa ili kuhalalisha tuhuma ambazo sasa zimedhihirishwa hazikuwa za kweli,”alisema Dkt. Masisi
Hivyo Serikali katika kipindi cha uchunguzi ilichukua hatua kadhaa kama Baba, ikiwa pamoja na Msajili kusimamisha huduma za Kanisa letu , kufunga ukumbi wa
na baadae kufuta usajili wa kanisa letu,” alisema na kuongeza “Mambo haya yote yalitokea kwa kipindi cha muda mfupi sana, na baada ya miezi sita, Jeshi la Polisi lilitoa majibu ya uchunguzi wao kwamba hatuna hatia.”
Alisema pamoja na majibu waliyopewa pia walipewa barua iliyowataka jengo lao la kanisa liweze kufunguliwa na kutumika kwa shughuli nyinginezo za kijamii na sio huduma za Kanisa.
Alisema Serikali ya Rais Samia ni sikivu na makini na ndiyo maana imewapa ruhusa kuendelea kumuabudu Mungu.
“Tunaishukuru Serikali yetu kwa kusimamia haki na kwa dhati, tunatoa tamko ya kuwa hatuna uhusiano wowote na wale wanaotetea mapenzi ya jinsia moja,”alisisitiza askofu huyo.
Pia alisema kanisa hilo kwa Sasa linasubiri rufaa ambayo walikata tangu Machi, mwaka huu hivyo Dkt. Masisi alieleza ana imani Serikali ya Rais Samia itaweza kujibu.