Serikali mjini Naivasha imeamuru kufungwa kwa kanisa lenye utata kutokana na madai ya vifo vya watoto wanne kutokana na wazazi kukosa kuwapeleka hospitalini kutokana na imani zao za kidini.
Kanisa linalojulikana kama “Church of God” katika eneo la Maella mjini Naivasha lilikuja kuangaziwa baada ya waumini wake watatu kukamatwa kufuatia malalamiko ya umma baada ya kukataa kuwapeleka watoto wao waliokuwa wagonjwa hospitalini kwa madai ya imani zao za madhehebu.
Mwaka huu pekee, watoto wanne wanadaiwa kufariki dunia kutokana na kutelekezwa na wazazi wao baada ya kujisikia vibaya na baadaye kufariki dunia huku watatu kati yao wakiripotiwa kuzikwa katika viwanja vya kanisa hilo.
Sasa, Naibu Kamishna wa Naivasha Mutua Kisilu ameagiza kanisa hilo kufunga milango yake hadi polisi watakapokamilisha uchunguzi wao kuhusu madai ya kifo na kutotimiza wajibu wa wazazi.
Kisilu alisema polisi wamezindua msako mkali wa kumtafuta mchungaji wa kanisa hilo ambaye amekimbia eneo hilo baada ya wananchi kutaka akamatwe kufuatia tuhuma za kuwafunza waumini wa dhidi ya kutafuta huduma za afya.