Kanisa moja nchini Uganda ‘Phaneroo Ministries International‘ limeweka Rekodi ya Dunia ya Guinness kwa kupiga makofi kwa muda mrefu zaidi baada ya waumini wake kupiga makofi bila kukoma kwa zaidi ya saa tatu.
“Kutaniko lilipiga makofi kwa jumla ya saa tatu dakika 16, likidumisha sauti ya wastani ya 88.5 dB. Ili jaribio liwe halali, ilibidi zibaki zaidi ya 80 dB kwa muda wote,” Guinness World Records ilisema katika taarifa.
Tukio hilo lililopewa jina la “Clap For Jesus”, katika ukumbi katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, liliandaliwa tarehe 30 Julai na kanisa la Phaneroo Ministries katika kusherehekea mwaka wake wa tisa.
Grace Lubega, kiongozi wa kanisa hilo, aliiambia Guinness World Records kuwa tukio hilo lililenga kuwaunganisha watu katika kushukuru na kusherehekea.
Washiriki 926 walitakiwa kupiga makofi mfululizo na wasimamizi waliwaondoa wale waliositisha.
Tukio hilo lilitiririshwa moja kwa moja na kufuatiliwa na waangalizi kutoka shirika la viwango la Uganda na bodi ya taifa ya kusimamia mpira wa vikapu.
Kundi hilo lilipindua rekodi ya hapo awali ya saa mbili na dakika tano, iliyowekwa na Clark Stevens na Tamasha la Uajabu nchini Uingereza mnamo 2019.