Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, Martin Griffiths, alisema Jumanne kwamba karibu watu milioni 16.7 nchini Syria wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Griffiths alitoa maoni yake katika mkutano maalum kuhusu Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Amefahamisha kuwa tetemeko la ardhi la Turkiye ni mojawapo ya matetemeko makubwa zaidi kuwahi kutokea duniani katika karne moja, akibainisha kuwa maafa hayo yaligharimu maisha ya maelfu ya watu katika nchi za Turkiye na Syria.
Hata hivyo amefahamisha kuwa athari za tetemeko la ardhi ni kubwa zaidi nchini Syria kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea huku akisisitiza haja ya kujengwa upya huduma za msingi na makazi.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa hali nchini Syria imekuwa mbaya zaidi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu ni sawa na robo tatu ya watu wote.