Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo, amewataka vijana wa Afrika, hususan kutoka Kusini mwa Afrika, kujitambua na kuwa tayari kuzitumikia nchi zao kwa weledi, uwezo na uzalendo mkubwa usiotiliwa shaka, hasa katika kuendeleza agenda ya kuongoza mapambano ya ukombozi wa kiuchumi kwa ajili ya wananchi ambao vyama vyao vilivyoko madarakani vimepewa dhamana ya kuwaongoza na kuwatumikia.
Katibu Mkuu Chongolo ameyasema hayo leo Alhamis, Juni 8, 2023, wakati akifungua Mafunzo ya Viongozi Makada wa Vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2023 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (MJNLS) iliyopo Kibaha kwa Mfipa, mkoani Pwani.
“Ukombozi wa mataifa yetu ulishafanyika na mataifa yetu yapo huru, harakati za ukombozi wa mataifa yetu Kusini mwa Afrika zilishaisha, sasa tuna wajibu wa kupambana na ukombozi wa kiuchumi na wa maisha bora ya wananchi tuliopewa dhamana ya kuwaongoza,” alisema Chongolo.
Pamoja na mambo mengine Ndugu Chongolo amewataka vijana kutambua wajibu wa kuiandaa kesho njema haswa kwa nyakati na mazingira ya sasa, ambapo wanatakiwa kujitambua na kubeba dhima ya uongozi unaolenga kuwatumikia watu kwa weledi na uzalendo mkubwa wa hali juu, kwa ajili ya kubadilisha na kuboresha hali za maisha ya watu.
Mafunzo hayo yatakayofanyika kwa takriban wiki mbili, yanajumuisha viongozi na makada wa Vyama vya MPLA, SWAPO, FRELIMO, ANC na ZANU PF, CCM pamoja na CPC.