Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema ameshangazwa na mashambulizi yanayoendelea Gaza dhidi ya raia na kusikitishwa na kushambuliwa kwa jengo moja lililokuwa na ofisi kadhaa za mashirika ya habari ya kimataifa.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema Guterres amefadhaishwa na shambulizi la anga la Israel lililofanywa jana katika jengo hilo.
Amesema Guterres pia anasikitishwa na mauaji ya raia, ikiwemo vifo vya watu 10 wa familia moja pamoja na watoto vilivyotokea katika shambulizi la usiku wa Ijumaa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo kuujadili mzozo kati ya Israel na Palestina. Wakati huo huo, viongozi wa ulimwengu leo wameelezea wasiwasi wao baada ya mashambulizi hayo ya Israel ambayo yamewaua pia watoto wanane.
Aidha, jeshi la Israel limesema leo kuwa kundi la Hamas limefyatua makombora kuelekea Israel.