Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za makusudi za kuzuia kuenea kwa matumizi mabaya ya zana za teknolojia ya akili mashine (AI), huenda teknolojia hiyo ikageuka uharibifu usiodhibitika.
Antonio Guterres alitoa indhari hiyo jana Jumatatu na kusisitiza kuwa, kuna haja kwa dunia kuunda mifumo na sheria za kuzuia matumizi mabaya ya teknolojia hiyo ya Artificial Intelligence.
Guterres ameeleza bayana kuwa, kuna udharura wa kubuniwa kanuni na miongozo kwa serikali, kampuni za teknolojia, na mashirika ya matangazo ya biashara ili yaweze kudhibiti uenezaji wa taarifa za urongo, za chuki na matumizi mabaya ya teknolojia ya akili bandia.
Amesema anapanga kuunda Bodi ya Ushauri ya Kisayansi ndani ya siku chache zijazo, na Bodi ya Ushauri ya Akili Mashine kufikia Septemba mwaka huu, ili ziandae ramani ya njia na muelekeo utakaochukuliwa na UN juu ya kadhia hiyo.
Onyo la Katibu Mkuu wa UN limekuja wiki chache baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutahadharisha pia kuhusu hatari ya matumizi mabaya ya akili mashine (AI).
Alisema hana mamlaka ya kuunda wakala kama wa IAEA hiyo ni juu ya majimbo 193 ya shirika hilo.
AI inaweza kudhuru afya ya mamilioni na kusababisha tishio la kuwepo kwa ubinadamu, madaktari na wataalam wa afya ya umma wamesema huku wakitoa wito wa kusitishwa kwa maendeleo ya akili ya bandia hadi idhibitiwe.
Akili bandia ina uwezo wa kuleta mapinduzi katika huduma ya afya kwa kuboresha utambuzi wa magonjwa, kutafuta njia bora za kutibu wagonjwa na kupanua huduma kwa watu wengi zaidi.
Lakini ukuzaji wa akili bandia pia kuna uwezekano wa kuleta athari mbaya za kiafya, kulingana na wataalamu wa afya kutoka Uingereza, Marekani, Australia, Costa Rica na Malaysia wakiandika katika jarida la BMJ Global Health.