Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kuzuiwa kwa malori ya misaada yaliyoko katika upande wa Misri wa mpaka na Ukanda wa Ghaza, akiielezea hatua hiyo kuwa inasababisha “ghadhabu ya kimaadili.”
Akiwa katika ziara yake katika kivuko cha mpaka cha Rafah jana Jumamosi, Guterres amesisitiza udharura wa utawala wa Israel kudhamini upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila kikomo katika eneo lote la Ghaza na kutoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano kwa sababu za kibinadamu.
Katibu Mkuu wa UN amesema: “hapa kutoka kwenye kivuko hiki, tunaona huzuni na uchungu wa yote hayo. Msururu mrefu wa malori ya misaada yaliyozuiwa upande mmoja wa malango na kivuli kirefu cha njaa kwa upande mwingine. Hiyo ni zaidi ya janga. Ni hasira ya kimaadili.”
Akiwa katika safari hiyo ya kutembelea kivuko cha Rafah, Guterres ameonya juu ya matokeo mabaya ya kuendelea kuzuiwa misaada, akisema, “ni wakati wa kuimimina misaada ya kuokoa maisha Ghaza.
Chaguo liko wazi: ama kuongezeka au ni njaa.”
Ziara hiyo ya Katibu Mkuu wa UN inafanyika sambamba na kuongezeka mashinikizo ya kimataifa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuutaka uruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Ghaza, ambayo iko katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji.