Umoja wa Mataifa umelezea wasiwasi wake Jumapili kuhusu mapigano yanayoendelea kati ya Vikosi vya Jeshi la Sudan na wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko Darfur Kaskazini.
Farhan Haq msemaji wa Umoja wa Mataifa, amesema katika taarifa kwamba, Katibu Mkuu Antonio Guterres amesikitishwa sana na hali inayoendelea huko El Fasher, Darfur Kaskazini, ambako mapigano makali yameripotiwa kati ya Vikosi vya Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF pamoja na wengine wanaohusika katika mapambano ya silaha.”
Ameongeza kuwa mapigano haya yana madhara makubwa kwa raia.
Haq amesema mapigano hayo pia yatazidisha mahitaji ya kibinadamu ndani na karibu na El Fasher wakati ambapo hali ya njaa imethibitishwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam kusini mwa El Fasher na kuna uwezekano mkubwa katika maeneo mengine ya watu kuhama katika mji huo.
Msemaji huyo ameongeza kuwa: “Katibu Mkuu anatoa wito kwa pande zote kutii wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu ya kulinda na kuruhusu kupita kwa usalama raia na kuwezesha ufikiaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo.”
Akirejelea wito wake wa kusitishwa mara moja uhasama na usitishaji mapigano wa kudumu, Haq amesema kuwa Guterres pia amezitaka pande hizo kurejea kwenye mazungumzo ya kisiasa kama njia pekee ya kufikia suluhu iliyojadiliwa.