Katibu mkuu wizara ya katiba na sheria Bi Mary Makondo amewataka maafisa uchunguzi waandamizi kutoka mamlaka mbalimbali za uhifadhi na za kisheria kutunza siri za wananchi watakaokwenda kutoa taarifa za kiuhalifu ili kusiwe na woga wowote kufanikisha kudhibiti matukio ya kiuhalifu.
Katibu Mkuu Makondo alisema hayo mjini Morogoro wakati akizungumza na maafisa uchunguzi waandamizi kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali, Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori nchini TAWA, Mamlaka ya hifadhi za taifa TANAPA na Wakala wa huduma za misitu nchini TFS.
Wadau hao walikuwa wakipitia sheria na kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi alizosema zinalenga kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu kwa kuwatambua na kuwalinda watoa taarifa na mashahidi na akasema uadilifu na uaminifu katika utunzaji wa siri ni mujibu wa viapo vyao.
“Kanuni zimefafanua kwa kina kwamba wale ambao taarifa zao zitafanikisha kuokoa Mali ya umma, kupatikana kwa wahalifu na kulinda mazingira na maisha ya binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa kufanyika, wamewekewa utaratibu wa kupatiwa motisha ikiwa ni pamoja na kuwafidia wake wote watakaoathirika kutokana na taarifa walizotoa”Alisema Katibu Mkuu Makondo.
Akasema maafisa hao wa uchunguzi waandamizi Ili waweze kuzifahamu na kutekeleza sheria hiyo ya ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi sura ya 446 na kanuni hizo kwa ufanisi zaidi na akawasisiza kuwa na lugha rafiki kwa mashahidi na watoa taarifa.
Akasema kutokana na uwepo wa sheria na kanuni hizo, wananchi hawatakiwi kuwa na woga kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu na matendo ya aina zote yanayofanywa kinyume na sheria kwani taarifa hizo zitakuwa Siri ana zitafanyiwa kazi bila kuwataja watoa taarifa.
Aidha mashahidi watakapotakiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, akawasihi wasiigope kwani kanuni hizo zitawalinda dhidi ya changamoto zote za kiusalama na nia kubwa ya sheria na kanuni ni kuhamasisha wananchi watoe taarifa za uhalifu unaotokea au unaotarajiwa kutokea katika jamii inayotakiwa iwe sehemu salama ambayo Kila Mwananchi ataishi kwa amani na utulivu.
“Muwalinde sana watoa taarifa kwasababu mkiwaanika wahalifu nao watawalipizia kisasi, na huwa hawana hofu kwenye hilo”
Mkurugenzi msaidizi wa ufuatiliaji haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Beatrice Mpembo, waliowezeshwa kutunga kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi, na washirika wa maendeleo Serikali ya Uingereza FCDO na Umoja wa ulaya, kupitia program endelevu ya kupambana na rushwa BSAAT, kutoka ofisi ya Rais Ikulu,akasema lengo la sheria hiyo ni kuimarisha utawala Bora na mapambano dhidi ya uhalifu.
Akasema sheria na kanuni hizo zitarahisisha utekelezaji wa sheria husika kuwa yenye tija na ufanisi mkubwa Ili kuwezesha haki kutendeka kwa wakati katika jamii na kutoa ulinzi wa kisheria wote wanaotoa taarifa za uhalifu wa makosa mbalimbali wanayoshuhudia yakitendeka kwenye jamii.
Mratibu wa program endelevu ya kupambana na rushwa, BSAAT, kutoka ofisi ya Rais, Ikulu,.Dkt Boniventure Baya, akaipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa namna wanavyogusa makundi muhimu kuifahamu sheria na kanuni hizo ikiwemo waandishi wa habari na maafisa uchunguzi ambao wataelimisha jamii na kupokea taarifa kwa maslahi ya nchi.
Naye mwakilishi wa washirik, Wakili wa Serikali kutoka NPS, Bi Florida Wenceslaus,akaahidi watalinda viapo vyao kwa kulinda Siri za watoa taarifa na mashahidi, kwani mara kadhaa KUMEKUWA na changamoto ya kupatikana ushahidi kutokana na mashahidi kuwa waoga lakini sasa sheria inawalinda.
Kanuni hizo mpya zilizopitishwa Januari mwaka huu zinaruhusu Mwananchi kumpatia taarifa za kiuhalifu kiongozi yeyote kuanzia ngazi za vijiji na mitaa, kata, wilaya, mkoa na faida, wakiwemo wa kiserikali na wa dini na hata vyombo vya habari ilimradi kwa mtu ambaye mtoa taarifa atamuamini na kufikishwa kwa mamlaka husika kwaajili ya kufanyiwa Kazi ambapo kanuni zimeweka taratibu za kuwalipa au kuwapa fidia kutokana na ama taarifa walizotoa au kuhusika katika kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu.
Wadau wanaopatiwa mafunzo pia wamekuwa wakishauri maoni mbalimbali kuboresha kanuni ama sheria hiyo.