Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema Wafanyabiashara wote katika eneo la mkoa wa kodi Kariakoo wanapaswa kusajiliwa na kupewa namba ya utambulisho wa Mlipa kodi (TIN) ndani ya siku kumi na tano tangu tarehe ya kuanza kwao biashara ambapo hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha sheria ya mwaka 2015 ya usimamizi wa kodi.
Taarifa iliyosainiwa na Kamishna Mkuu wa TRA Alphayo Kidata, imeeleza kwamba kuanzia tarehe ya kutolewa kwa taarifa hii Mfanyabiashara yoyote atakayeendesha biashara yoyote katika eneo la Kariakoo bila kuwa na TIN na kutumia mashine ya kutolea risiti ya EFD atakua ametenda kosa kisheria litalopelekea adhabu, kifungo au vyote kwa pamoja.
“TRA itaendesha zoezi maalum katika eneo la Mkoa wa Kodi Kariakoo kuhakikisha kuwa sheria na taratibu za uendeshaji biashara kama ilivyoelezwa katika taarifa hii zinafuatwa, Wafanyabiashara wote kwenye mkoa wa kodi wa Kariakoo na maeneo yote nchini wanahimizwa kuzingatia sheria na kujiepusha na usumbufu, yeyote anayetaka maelezo zaidi atupigie kwenye namba ya bure 0800750075 au whatsapp 0744233333”