Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (Mb), leo Aprili 24, 2024 amewasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 katika Mkutano wa Kumi na Tano Kikao cha Kumi na Tatu.
Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi
1.Serikali itaendelea kusimamia na kuendeleza Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi kwa kuchukua hatua mbalimbali, lengo likiwa ni kuhakikisha mchango wa Sekta hii katika maendeleo ya Taifa letu unaimarika.
2. Serikali itaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati na kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka kitalu cha Ruvuma (Ntorya) hadi Madimba lenye urefu wa kilomita 34.2 na uwezo wa kubeba futi za ujazo milioni 140 kwa siku.
3. Aidha, Serikali inatarajia kukamilisha majadiliano ya Mikataba ya mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia Kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG) ili utekelezaji wake uanze.
4.Serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa Gesi Asilia katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kufanya tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, usanifu wa kihandisi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwenye viwanda vya Mkuranga pamoja na Kongani ya Viwanda ya Kwala Mkoani Pwani.