Dunia inakwenda kasi, na teknolojia inazidi kuimarika watu wanahabarika kupitia mitandao ya kijamii.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zinazofanya vizuri katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
Na hii inachagizwa na ongezeko la watumiaji wa simu janja na huduma ya mtandao (intaneti) nchini.
Mitandao hii si tu majukwaa ya kimawasiliano, bali ni fursa katika ulimwengu wa leo ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla endapo itatumika vizuri.
Licha ya kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa huduma za intaneti na simu janja, lakini matumizi ya mitandao ya kijamii yameendelea kuwa kitendawili kwa Watanzania wengi.
Wapo ambao wamekuwa wakiitumia mitandao hiyo kwa namna sahihi ambayo imekuwa ikiwanufaisha kama vile kibiashara, kikazi na kielimu na wale ambao wamekuwa wakiitumia ndivyo sivyo.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumeshuhudiwa kukithiri kwa matukio ya upotoshwaji wa taarifa, usambazaji wa maudhui yasiyo na maadili (picha na video za utupu na lugha za matusi) na udhalilishaji yanayofanywa mitandaoni.
Hii inaashiria kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na kuwepo kwa kundi kubwa la Watanzania ambao hawajui kutumia mitandao hiyo kwa malengo ya kunufaika.
Ikumbukwe kuwa matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii yana athari kubwa kwa ustawi wa jamii ya sasa na hata baadaye kwa kuwa maudhui yanayopandishwa katika majukwaa hayo zinadumu vizazi kwa vizazi.
Kupitia programu ya #KEEP IT ON inayofanywa na ZAINA FOUNDATION inatoa nafasi ya kutoa elimu kwa umma umuhimu wa matumizi ya mitandao sambamba na vyombo vya habari kupaza sauti kuhusiana na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na ushiriki bora katika kujifunza juu ya matumizi bora ya mitandao ya kijamii.