Kenya itaanza mpango wa dharura wa chanjo ya polio tarehe 24 Agosti, wiki kadhaa baada ya kugunduliwa kwa visa vya polio katika eneo la kaskazini-mashariki mwa nchi.
Kampeni ya chanjo hiyo inalenga watoto milioni 7.4 walio na umri wa chini ya miaka mitano na itaweka kipaumbele katika kaunti 10 zilizo katika hatari kubwa, ikiwa ni pamoja na kaunti ya Garissa, ambapo mlipuko wa hivi karibunui ulitokea.
Takribani 3% ya watoto wa Kenya hawajachanjwa dhidi ya polio, Mkurugenzi mkuu wa afya wa Kenya Dkt Patrick Amoth alisema katika mkutano na wanahabari Jumanne.
Kenya ilitokomeza virusi ‘wild poliovirus’ , aina ya polio iliyoenea zaidi, mwaka wa 2014.
Hata hivyo, mwezi Julai, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilionya kuwa Kenya inakabiliwa na hatari kubwa ya kusambaza polio inayotokana na aina ya virusi vya polio ambayo huathiri jamii zisizo na chanjo.
WHO ilisema kuwa hatari ya polio nchini Kenya ni kubwa zaidi katika kambi za wakimbizi nchini humo, ambazo mara nyingi zina msongamano wa watu na zina vifaa duni vya vyoo, viwango vya juu vya utapiamlo na harakati za mara kwa mara za watu nchini Somalia, ambayo imekuwa na milipuko ya hivi karibuni ya polio.