Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Masuala ya Diaspora, Roseline Njogu, ameviambia vyombo vya habari kwamba licha ya kufungwa anga ya Sudan, nchi hiyo imeunda timu ya kiufundi ya mashirika mbalimbali ambayo inafuatilia hali inavyoendelea nchini Sudan.
“Tunakusanya vifaa vyote vinavyohitajika ili kuwahamisha raia wetu mara tu anga ya Sudan itakapokuwa wazi na kukawepo uwezo wa kuwahamisha watu kwa usalama,” Njogu amesema.
Mapigano ya kuwania madaraka baina Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kamanda wa vikosi vya jeshi la taifa ambaye pia ni mtawala wa Sudan, na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, mkuu Vikosi vya Msaada wa Dharura (RSF) yalizukak tarehe 15 mwezi huu wa Aprili mjini Khartoum na kuenenea katika miji na majimbo kadhaa ya nchi hiyo.
Majenerali hao wawili ni washirika wa zamani kwani walishirikiana kutekeleza mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Masuala ya Diaspora wa Kenya, Roseline Njogu, amesema nchi hiyo imejitolea kuhakikisha raia wake wote wanaokolewa salama na kurudishwa nyumbani ikiwa maisha yao yamo hatarini au katika hatari ya janga la kibinadamu.
Taasisi za kikanda zikiwemo Umoja wa Afrika, kundi la kikanda la IGAD, na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), zimesema zinazungumza na mahasimu mbalimbali hasa majenerali hao wawili, kujaribu kusitisha mapigano.
Mapema wakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes, amesema watu 185 wameuawa na wengine 1,800 kujeruhiwa katika mapigano ambaye yanaendelea kwa muda wa siku nne sasa kati ya pande zinazohasimiana nchini Sudan.