Awamu nyingine ya mazungumzo ya kujaribu kupata muafaka kati ya Serikali ya Kenya na upinzani, inatarajiwa kuendelea tena hivi leo kukiwa na matumaini ya kupatikana makubaliano.
Baada ya wiki kadhaa za maandamano ya upinzani, kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na shinikizo za kuifanyia marekebisho Tume ya Uchaguzi.
Kikao hiki kinaendelea kuratibiwa na rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, yanatarajiwa kutoa suluhu ya mvutano unaoendelea kati ya kinara wa upinzani Raila Odinga na Serikali, ambapo kila upande ulichagua timu ya watu watano.
Muungano wa upinzani Azimio uliongoza maandamano mwezi Machi na Julai dhidi ya utawala wa rais William Ruto kupinga kile walichosema ni kupanda kwa gharama ya maisha na kutaka mageuzi katika tume ya uchaguzi kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.
Makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humo yanasema karibia watu 30 walifariki katika maandamano hayo wakati upinzani ukisema rekodi zake zilionyesha watu 50 waliuawa.
Upinzani ulisimamisha maandamano mwezi Aprili na Mei ili kuruhusu mchakato sawa wa mazungumzo ya pande mbili, lakini maandamano yalianza tena baada ya mazungumzo kuvunjika.