Mfalme wa Uingereza, Charles wa tatu anatarajiwa kutamatisha ziara yake nchini Kenya kwa kukutana na viongozi wa dini katika jiji la Pwani la Mombasa, ambalo amekuwa akizuru kuanzia hapo jana.
Kabla ya mkutano huo, Mfalme Charles atatembelea Kanisa Kuu la Angilikana, na baadaye kukutana na viongozi hao wa dini kujadiliana nao kuhusu kazi zao za kuimarisha amani, usalama na maendeleo, Pwani ya nchi hiyo.
Jana, Mfalme huyo alizuru kambi ya wanajeshi wa majini ya Mtongwe, kujionea mafunzo yaliyotolewa na wanajeshi wa Uingereza kwa wenzao wa Kenya, kuhusu namna ya kupambana na adui majini
Kabla ya kwenda Mombasa, Mfalme Charles alizuru jiji kuu Nairobi kwa siku mbili na kukiri madhila yaliyofanywa na serikali za kikoloni, lakini hakuomba msamaha licha ya kupokea shinikizo kutoka kwa wanaharakati mbalimbali.