Kenya na Somalia siku ya jumatatu zimekubaliana kufungua tena vituo vitatu vya mpaka kati ya nchi hizo mbili baada ya kufungwa kwa miaka 12 kutokana na ukosefu wa usalama na vitisho vinavyohusiana na ugaidi.
Ujumbe wa mawaziri watatu kutoka serikali ya shirikisho la Somalia uliowasili Kenya umekutana na waziri wa usalama wa Kenya Kithure Kindiki ambapo walikubaliana kufungua mpaka wa Mandera/Bulahawa jimbo la Mandera, mpaka wa Kiunga/Ras Kamboni, jimbo la Lamu na Liboi-Harhar/Dhobley jimbo la Garissa, ambayo ilifungwa na utawala wa Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta mnamo 2011.
Hatua ya kufungwa kwa mpaka ilitokana na uvamizi wa mara kwa mara na mashambulizi yaliyopangwa na kundi la kigaidi la al Shabaab, na kusababisha Kenya kutuma jeshi lake Somalia kuzuia mashambulizi zaidi.
Katika mkutano huo wa ngazi ya juu wa mawaziri, Kindiki alikutana na Waziri wa Usalama wa Ndani, Serikali ya Shirikisho la Somalia Mohamed Ahmed Sheikh Ali, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Abdulkadir Mohamed Nur na Abshir Omar Jama, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, katika ofisi ya rais jijini Nairobi.
Pamoja na kuwa mipaka hiyo ilifungwa rasmi wakati huo, wahalifu na wahamiaji bado wamekuwa wakitumia hususani wanamgambo wa al-Shabaab walio na makao yao nchini Somalia.
Katika mkutano huo wa mawaziri wa nchi hizo mbili umelenga kufungua mipaka hiyo kwa lengo la kuimarisha usafiri wa watu na bidhaa pamoja na kudumisha na kukuza ushirikiano wa kikanda, na maendeleo endelevu kati ya nchi hizo.
Mkutano huo pia ulilenga kudhibiti uhamiaji usio wa kawaida, uhalifu na itikadi kali za kigaidi na pia kurahisisha mahitaji ya visa, na ufanyaji wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili jirani kama anavyoeleza Mohamed Ahmed Sheikh Ali, waziri wa Usalama wa Ndani, Serikali ya Shirikisho la Somalia.
Kenya na Somalia zina mpaka wa nchi kavu wenye urefu wa kilomita 680 (maili 420) na zimekuwa kwenye mzozo wa muda mrefu kwa miaka mingi kuhusu eneo linaloweza kuwa na utajiri wa mafuta na gesi katika Bahari ya Hindi.
Chanzo:.VOA